Programu ya Usimamizi wa Fedha za Umma
Programu ya Utawala wa Fedha za Umma ilianzishwa mwaka 2016. Dhamira yake ni kuhamasisha utawala bora wa fedha na utendaji kwenye anuwai ya maeneo kama sera ya mapato na utawala, mchakato wa kuandaa bajeti, usimamizi wa matumizi, pamoja na ukaguzi na uangalizi.
Sikika inafanya uraghabishi wenye ushahidi ambao hutoa nafasi kwa wananchi kushiriki katika uundaji wa sera, mipango ya maendeleo na bajeti; kufuatilia manunuzi sahihi ya umma na utoaji wa huduma; na kuimarisha uwajibikaji kupitia ukaguzi wa nje na michakato ya usimamizi wa Bunge. Kazi yetu pia inahakikisha kuwa Mpango wa Marekebisho ya Usimamizi wa Fedha za Umma ni sikivu na unawajibika kwa jamii kwa kuwafanya wananchi kujua changamoto zilizopo na vikwazo vya usimamizi mzuri wa fedha za umma na kuwafanya wananchi waelewe ni kwanini juhudi za mageuzi zinazofanywa na Serikali ni muhimu kwa maendeleo ya kitaifa.
Ukusanyaji wa Mapato
Uhamasishaji wa rasilimali za ndani ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya Tanzania. Lengo letu la kwanza ni kuboresha makadirio na ukusanyaji wa mapato mzuri, na wenye usawa. Sikika inahakiki na kutathmini sera, sheria, na kanuni za mfumo wa kodi ili kubaini vizuizi kwenye ukusanyaji wa mapato na fursa za kupanua wigo wa kodi. Tunafanya kazi na mamlaka ya mapato katika ngazi ya serikali kuu na serikali za mitaa pamoja na vikundi vya walipa kodi ili kubaini fursa za mapato na vichocheo vya ulipaji kodi kwa hiari pamoja na kukuza utamaduni wa kitaifa wa kulipa kodi.
Mipango na Bajeti
Lengo letu la pili ni kuhimiza fedha za umma zipangwe na kutumiwa kwa ufanisi, usahihi na uwazi zaidi. Sikika inafanya kazi na Wizara ya Fedha na Mipango kutathmini njia bora za udhibiti wa matumizi na hatua za kupunguza gharama zinazoweza kuepukika kupitia mchakato mzuri wa kuandaa bajeti. Pia tunafanya uraghabishi katika kuhakikisha uwazi, ufanisi, na usawa katika uhamishaji wa fedha serikali kuu kwenda kwa serikali za mitaa ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wanafurahia upatikanaji wa huduma muhimu za umma. Tunafanya kazi na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma kuimarisha jukumu la wananchi katika usimamizi wa manunuzi ya umma katika ngazi ya jamii. Sikika pia inafanya kazi na Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika kufanya Utafiti wa Uwazi wa Bajeti katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (SN OBS) ambao unapima viwango vya uwazi katika utekelezaji wa bajeti na na ushiriki wa wananchi katika ngazi ya serikali za mitaa.
Uangalizi na Usimamizi wa Fedha
Lengo letu la tatu ni kuboresha uzingatiaji wa udhibiti na usimamizi mzuri wa fedha. Sikika inashirikiana na Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani kuunda mkakati wa kitaifa wa ukaguzi wa ndani ili kuimarisha ufanisi wa udhibiti wa ndani katika ngazi ya serikali za mitaa. Pia tunahimiza ufanisi wa kamati za uangalizi za bunge katika kufuatilia utekelezaji wa wakati wa mapendekezo ya ukaguzi wa nje ili kuzuia hatari zisizo za lazima za kifedha.
Vyombo vya Habari na Asasi za Kiraia
Lengo letu la nne ni kuweka mazingira ambapo vyombo vya habari na asasi za kiraia zinaweza kufuatilia kwa uhuru mijadala/midahalo na kukosoa utendaji wa serikali juu ya usimamizi wa fedha za umma na matukio ya usimamizi mbaya wa fedha yanayoripotiwa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Tunafanya tathmini ya sheria mbalimbali kama vile Sheria ya Mashirika yasiyo ya Serikali, Sheria ya Takwimu, Sheria ya Upatikanaji Habari, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ili kupata maeneo au sehemu zinazokwamisha upatikanaji wa taarifa, uhuru wa kujieleza, haki ya kushirikiana na haki ya kukusanyika kwa uhuru. Pia, tunafanya kazi na washirika wetu wengine; watunga sera na Wabunge kwa lengo la kuhamasisha kupitiwa kwa sheria ambazo zinapunguza ushiriki wa asasi za kiraia katika masuala ya usimamizi wa fedha za umma.

