Programu ya Afya
DAWA NA VIFAA TIBA
Sikika inafanya kazi kuboresha uwepo na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vyenye ubora kwa wananchi wote kupitia vituo vya kutolea huduma za afya vya serikali. Mbinu mbali mbali hutumika kufanya utetezi wa mipango na bajeti sawia kwa ajili ya dawa na vifaa tiba katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya. Vile vile, inahamasisha ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika ununuzi na usambazaji wa dawa na vifaa tiba.
Ili kuhakikisha lengo hili linafikiwa, Sikika hufanya tafiti juu ya ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya; ufuatiliaji wa uwepo na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba; mahojiano na mikutano pamoja na wadau ili kujua hali halisi iliyopo na kutathmini changamoto ambazo zinaweza kushughulikiwa kwa kuimarisha mifumo ya afya. Katika ngazi ya taifa, Sikika inashirikiana na Wizara ya afya maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Ofisi ya Rais – Tamisemi kwa kutoa mapendekezo kupitia vikundikazi vinavyoratibu maendeleo ya dawa, vifaa tiba pamoja na Teknolojia ya Afya.
UTAWALA NA USIMAMIZI WA FEDHA
Idara ya Utawala na Usimamizi wa Fedha za Afya inafanya kazi kufikia malengo makuu matatu; kuongeza ufanisi wa bajeti, uwazi na uwajibikaji ndani ya serikali kuu pamoja na serikali za mitaa.
Katika kufanikisha malengo hayo, tunafanyakazi kwa karibu na wadau wakuu ambao ni Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii ili kuchangia kuleta mabadiliko na kufikia malengo yaliyoainishwa.
Tunaamini kwamba uwazi katika bajeti utakuza ushiriki wa wananchi kuanzia kwenye mchakato mzima wa uandaaji wa bajeti na hivyo kuweka umiliki wa mchakato huo mikononi mwa wananchi.
Kukuza ufanisi katika mgawanyo na matumizi ya rasilimali ndani ya sekta ya afya pamoja na usimamizi mzuri, vitachangia utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wote.
RASILIMALI WATU – AFYA
Sikika inadhamiria kuona ongezeko la bajeti ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuajiri wafanyakazi wenye taaluma stahili, kuwagawa kwa uwiano kulingana na mahitaji ya kituo. Vile vile inatarajia kuona watumishi wanazingatia na kutoa huduma kulingana na maadili ya taaluma zao.
Sikika inafanya utafiti kuhusu uwepo wa watumishi, hususani ajira na mgawanyo wa wafanyakazi, kudumu kwao kazini na uzingatiaji wa maadili ya kazi. Tunajenga uwezo wa wananchi kufuatilia upatikanaji wa huduma za afya na jinsi wanavyoweza kushiriki katika na mijadala na watoa huduma za afya, watunga sera, watendaji wa serikali za mitaa na wabunge, katika masuala yanayohusu watumishi katika sekta ya afya. Katika ngazi ya taifa, tunashirikiana na watendaji wengine kupitia Kikundi kazi cha Rasilimali Watu pamoja na warsha na mikutano ya kitaalamu juu ya maendeleo ya watoa huduma za afya.

